Ubalozi  wa  Tanzania Nchini Mozambique unayo furaha kuwajulisha Watanzania wanaoishi Jamhuri ya Mozambique na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Maonyesho ya bidhaa za Tanzania Mozambique yaliyoandaliwa kwa pamoja kati ya TanTrade ya Tanzania, CTA ya Mozambique na Gavana wa Jimbo la Nampula Mheshimiwa Victor Borges.  Maonyesho hayo yatakayofanyika katika mji wa Nampula katika jimbo la Nampula kuanzia tarehe 20 hadi 25 Agosti, 2018.  

Jumla ya Makampuni ishirini na nane (28), Wilaya ishirini na tatu (23) na vikundi vya ujasiliamali thelathini (30) vitashiriki katika Maonyesho hayo ambayo yanafanyika kwa mara ya pili kufuatia Maonyesho kama hayo yaliyofanyika miaka sita iliyopita.

Lengo la maonyesho hayo ni kujenga na kukuza mahusiano na ushirikiano wa raia wa Nchi zetu mbili za Tanzania na Mozambique katika kujenga, kukuza na kuimarisha Uchumi ambao ni nyenzo muhimu sana katika kuimarisha  mahusiano ya raia wetu yaliyojengwa kipindi kirefu na waasisi wa Mataifa yetu mawili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Samora Moses Machel.

Sambamba na Maonyesho hayo, bidhaa kutoka katika Wilaya ishirini na tatu (23) zinazounda Jimbo la Nampula zitaonyeshwa ikiwa ni pamoja na bidhaa mbali mbali zinazozalishwa na Wananchi wa Nampula  kutoka Viwandani, na   hivyo kutoa fursa mbali mbali kwa Wananchi wa Nampula na Vitongoji vyake kujifunza, kubadilishana mawazo na kujenga mazingira ya kupanua wigo wa fursa za kibiashara kati na baina ya Washiriki katika Maonesho hayo.

Wananchi wa Nampula watumie fursa hii vizuri ya kushiriki na kupata fursa ya kupata Wabia wa ushiriki wa kibiashara.  Maonyesho haya, yataendelea kufanyika kila mwaka na kushirikisha Majimbo ya Cabo Delgado, Niasa na Tete.

Maonyesho haya tunataka yawe kichocheo madhubuti cha kukuza Mahusiano kwa upande mmoja na kuimarisha uwezo wa raia wa pande zetu mbili katika kupanua wigo na kujenga uwezo wa kibiashara katika maeneo ambamo fursa hazijabainishwa vyema, hazijatumika vilivyo na hivyo ni matumaini ya Watanzania kwamba Mazingira haya yakitumika vizuri yanaweza yakawa kichocheo kikubwa cha kukuza uwezo wa Wananchi wa pande hizi mbili Kiuchumi.  Aidha, kupitia Maonyesho haya mahusiano kati na baina ya Raia wa nchi hizi mbili yatakuzwa na kuimarishwa.

Maonyesho hayo yanatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 21 Agosti, 2018 na yatafungwa rasmi tarehe 25 Agosti, 2018.