Tarehe 5 Machi 2026, Mhe. CP.  Hamad K. Hamad, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji, amefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Nampula.Lengo la ziara hiyo ni kufanya majadiliano ya kitaalamu, kubaini maeneo ya ushirikiano ya pamoja na kuandaa mikakati ya kuanzisha na kuboresha ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji.
Katika ziara hiyo Mhe. Balozi amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu wa Serikali wa Mkoa huo ambaye amemwakilisha Gavana. Katika mazungumzo baina ya viongozi hao, Mhe. Balozi, alithibitisha dhamira Serikali ya Tanzania katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Serikali ya Msumbiji hususan katika nyanja za biashara, uwekezaji, miundombinu na usafirishaji wa bidhaa.
Vilevile, viongozi hao walijadili umuhimu wa kimkakati wa Bandari ya Nacala iliyopo mkoani humo na uwezekano wa kuanzisha ushirikiano wa taasisi kati ya Mamlaka ya Bandari ya Nacala na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA). Aidha, pamoja na mazungumzo hayo, Mhe. anatarajia kutembelea bandari hiyo ili kujionea fursa za ushirikiano zilizopo.
Sambamba na hayo Mheshimiwa Balozi alipata fursa ya kutembelea kiwanja cha ndege cha Nacala pamoja na kiwanda cha kuzalisha ngano cha Azam kinachomilikiwa na Mwekezaji wa Kitanzania.
Itakumbukwa kuwa, ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Msumbiji.