Tarehe 17 Agosti 2025 Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshiriki Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi na Serikali ambao ni Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Ivato, Antananarivo nchini Madagascar. Mkutano huo umebeba maudhui yanayosema _"Advancing Industrialisation, Agricultural Transformation, and Energy Transition for a Resilient SADC._"

Mhe. Dkt. Mpango ambaye aliwasili nchini Madagascar tarehe 15 Agosti, 2025 akimwakilisha Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huo, tarehe 16 Agosti, 2025 Mhe. Dkt. Mpango alishiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Organ Troika Summit).

Aidha, katika Mkutano Mkuu, Mhe. Emmerson Mnangagwa, Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe amekabidhi Uenyekiti wa SADC kwa Mhe. Andry Nirina Rajoelina, Rais wa Jamhuri ya Madagascar utakaodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja. Vilevile Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekabidhi uenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ Troika) kwa Jamhuri ya Malawi mara baada ya kuhitimisha uongozi wa mwaka mmoja wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ulioanza Agosti 2024.

Mkutano huo umejadili agenda kadhaa ikiwemo hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mpango Mkakati Elekezi wa kanda, kuanisha mafanikio na changamoto za utekelezaji. Utekelezaji umejikita katika nguzo kuu nne zikiongozwa na nguzo kuu ya Amani, Usalama na Utawala wa Kidemokrasia. Nguzo nyingine ni maendeleo ya viwanda na utangamano wa masoko, Maendeleo ya miundombinu katika kuchagiza utangamano pamoja na maendeleo ya kijamii na rasilimali watu.

Miongoni mwa mafanikio yaliyojadiliwa ambayo yamepatikana ni pamoja na kupungua kwa matukio ya ugaidi, kuimarika kwa demokrasia katika Kanda kupitia chaguzi huru na haki, kuongezeka kwa huduma za kifedha, kuongezeka kwa thamani ya mauzo ya bidhaa za viwanda na kuongezeka kwa miamala iliyofanyika kupitia mfumo wa malipo wa kikanda.