Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji uliadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani tarehe 7 Julai 2025. Tukio hilo lilihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wanadiplomasia, viongozi wa Serikali ya Msumbiji, walimu na wanafunzi wa lugha ya Kiswahili, pamoja na Watanzania wanaoishi Msumbiji.
Maadhimisho yalilenga kuonyesha nafasi ya Kiswahili kama lugha ya amani, mshikamano na maendeleo barani Afrika, hususan baada ya kutambuliwa rasmi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuwa lugha ya kimataifa.
Katika hotuba yake, Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji Mhe. Hamad Khamis Hamad, alisisitiza kuwa Kiswahili ni urithi wa kitamaduni na chombo cha kuimarisha ushirikiano wa kikanda, hususan kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ufundishaji wa Kiswahili katika shule na vyuo nchini Msumbiji na kwingineko.
Kulikuwa na burudani za muziki na maonesho ya picha mjongeo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo kuonesha utajiri wa lugha hii adhimu, tamaduni na rasilimali za nchi yetu. Katika hotuba yake Mhe Balozi Hamad, aliwaeleza wageni waalikwa kuwa Kiswahili ni lugha inayozungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 duniani, na ni lugha rasmi ya Umoja wa Afrika pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, Kiswahili ni nyenzo muhimu ya kudumisha mshikamano katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ambapo pia Msumbiji na Tanzania ni wanachama.
Kwa Tanzania, Kiswahili siyo tu lugha ya mawasiliano, bali ni nguzo ya utaifa wetu. Ni lugha iliyoongoza harakati za ukombozi barani Afrika, na sasa kinaendelea kuwa daraja la mawasiliano ya kiuchumi, kisiasa na kitamaduni.
Tanzania inafurahia kuona idadi ya wanafunzi wa Kiswahili katika shule na vyuo ikiongezeka, jambo linalodhihirisha kiu ya kujifunza lugha hii. Maadhimisho yalipambwa na ngoma za asili ya makonde na muziki kizazi kipya ambao unapendwa zaidi na wananchi wengi wa Msumbiji na eneo la uwakilishi. Kulikuwa na vyakula na vinywaji.
Shughuli hizo ziliwavutia wadau wengi zaidi ambao waliahidi kuenzi na kushirikiana katika safari ya kukuza Kiswahili.
Balozi aliwaeleza wageni kuwa, kila mmoja ashiriki kulinda, kukuza na kutangaza Kiswahili ili kiendelee kuwa chombo cha mshikamano wa kikanda na kimataifa. Ubalozi ulianzisha na unaendelea na darasa la Kiswahili kwa Wafanyakazi wa Redio Mozambique na unatarajia pia kuanzisha darasa kama hilo kwa Televisheni ya Taifa ya Msumbiji (TV Mozambique) ili kuongeza wigo wa wanaojifunza lugha hiyo.
Balozi alishatembelea katika vituo hivyo vya Habari na kuzungumza na Uongozi wa juu lengo likiwa ni kuenzi na kujenga mahusiano mazuri kati ya Kituo cha Utamaduni kinachotarajiwa kufunguliwa. Ubalozi uko kwenye hatua za mwisho kufungua Kituo cha Utamaduni kwa ajili ya kukuza lugha ya Kiswahili na urithi wa kitamaduni wa Tanzania. Kinachosubiriwa ni Kibali kutoka Wizara ya Utamaduni Msumbiji.
Katika maadhimisho hayo, Mhe Balozi Hamad alitoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake kubwa katika kuendeleza na kukuza Lugha ya Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji utaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza mafunzo ya Kiswahili na shughuli za kitamaduni zinazolenga kudumisha urithi huu adhimu.