Tarehe 15 Septemba 2025, Mhe. Hamad K. Hamad, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji alikutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Joaquim A. Chissano, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji.
Lengo la Mazungumzo hayo ni Mhe. Balozi Hamad kujitambulisha rasmi kwa Mhe. Rais Mstaafu Chissano, ikiwa ni mwendelezo wa hatua za Mhe. Balozi kukutana na Viongozi mbalimbali wa Serikali ya Msumbiji Pamoja na Jumuiya ya Wanadiplomasia waliopo nchini Msumbiji, zoezi ambalo amelifanikisha kwa kiasi kikubwa tangu alipowasili nchini Msumbiji mwezi Aprili 2025. Kadhalika, mazungumzo hayo yalilenga kuendeleza uhusiano wa kihistoria na kidugu uliopo kati ya Tanzania na Msumbiji.
Katika mazungumzo yao Mhe. Balozi Hamad alimshukuru Mhe. Chissano kukubali kufanya nae mazungumzo. Aidha, aliwasilisha salamu za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania wote kwa ujumla.
Mhe. Balozi alieleza kuwa Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu na chimbuko la uhusiano wa kihistoria na kidugu baina ya Tanzania na Msumbiji tangu kipindi cha kupigania uhuru wa Mataifa ya haya mawili. Hivyo, alimuhakikishia Mhe. Chissano kuwa Tanzania itaendelea kudumisha na kuimarisha uhusiano huo katika nyanja zote za kimaendeleo kama Diplomasia, Uchumi, Utamaduni, Ulinzi na Teknolojia.
Vilevile, Mhe. Balozi alipongeza juhudi za kimaendeleo zinazofanywa na Taasisi ya Joaquim Chissano Foundation ambayo ipo chini ya Mhe. Rais huyo Mstaafu ambapo Taasisi hiyo inashughulika na kukuza maendeleo endelevu, amani, na ustawi wa jamii za watu nchini Mozambique na Afrika kwa ujumla. Taasisi hiyo pia, inahusika na kuhamasisha utalii endelevu, uhifadhi wa mazingira, usalama wa wanyamapori, na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Sanjari na hayo, Mhe. Balozi alieleza mkakati wa Ubalozi kuhusu kufungua Kituo cha Utamaduni (Tanzania Culture Center) Ubalozini na kueleza kuwa mchakato wa kukamilisha taratibu ili kupatiwa kibali upo katika hatua nzuri. Aliongeza kuwa, kituo hicho pamoja na masuala mengine kitashughulika na kufundisha Lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wake Mhe. Chissano alipongeza hatua ya Mhe. Balozi kuona umuhimu wa kumtembelea ili kujadili masuala mbalimbali yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Msumbiji. Mhe. Chissano alieleza kuwa anaamini Mataifa haya sio tu yana historia ya muda mrefu ya ujirani bali ni udugu kutokana na muingiliano mkubwa wa jamii za pande zote mbili.
Mhe. Chissano alitoa historia na chimbuko la Mataifa haya tangu kipindi cha kupigania uhuru wa Tanzania na Msumbiji na kutambua mchango wa viongozi waasisi wa Mataifa haya mawaili ambao ni Hayati Mwl. Julius Nyerere wa Tanzania na Hayati Samora Machel wa Msumbiji. Lakini pia amepongeza ushirikiano ulioendelea kuenziwa na Awamu zote za uongozi kwa upande wa Tanzania na Msumbiji.
Aidha, alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ikiongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia katika kushughulikia masuala mbalimbali ya kimaendeleo vilevile, katika kutatua changamoto mbalimbali kwa njia ya amani ambapo amemwelezea kuwa ni kiongozi shupavu ambaye ni miongoni mwa Marais Wanawake wachache barani Afrika.
Sanjari na hayo, Mhe. Chissano alipongeza dhamira ya Ubalozi kuhusu kufungua Kituo Cha Utamaduni Ubalozini na kuahidi kuunga mkono juhudi hizo kupitia Taasisi yake ya Joaquim Chissano Foundation.
Mazungumzo baina ya Mhe. Balozi Hamad na Mhe. Rais Mstaafu Chissano yamekuwa na mafanikio na yanatoa mwanga wa kuendeleza juhudi zinazo fanywa na Ubalozi katika kuimarisha Uhusiano katika nyanja zote za kimaendeleo kama upande wa Utamaduni kupitia juhudi za kubidhaisha na kukuza Lugha ya Kiswahili nchini Msumbiji.
Imetolewa na:
UBALOZI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA MAPUTO, MSUMBIJI
SEPTEMBA 2025.
