Tarehe 11 na 12 Februari, 2026, Mhe. Hamad K. Hamad, Balozi wa Tanzania nchini alihudhuria Mkutano wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Kidigitali nchini Msumbiji. Mkutano huo uliandaliwa na Wizara ya Mawasiliano na Mabadiliko ya Kidigitali (MCTD) katika ukumbi wa Indy Village na kufunguliwa rasmi na Mheshimiwa Daniel Francisco Chapo, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji.
Mkutano huo ulilenga kuharakisha uboreshaji wa utawala wa umma chini ya kaulimbiu isemayo: “Kuelekea Dola ya Kisasa, ya Kidigitali na Inayomweka Mwananchi Mbele.”
Serikali ilizindua rasmi toleo jipya lililoboreshwa la mfumo wa visa ya kielektroniki na Electronic Travel Authorization (ETA), unaoendeshwa kwa ushirikiano na VFS Global, kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za usafiri kwa watalii na wafanyabiashara.
Mkutano huo uliwakutanisha wadau kutoka sekta ya umma, sekta binafsi na washirika wa kimataifa ili kuratibu juhudi katika utawala wa kidigitali, ujumuishaji wa kifedha, na maboresho ya utoaji wa huduma za umma.
