Mhe. Daniel Baran Sillo (Mb.), Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibian na Pasifiki (OACPS) kwa ngazi ya Mabunge ya Kanda ya Afrika (African Regional Parliamentary Group), pamoja na Mkutano wa Kwanza wa Bunge la Afrika na Umoja wa Ulaya (Africa–EU Parliamentary Assembly – AEPA), inayofanyika kuanzia tarehe 7 hadi 14 Mei, 2026 nchini Ufalme wa Eswatini.
Katika ziara hiyo, Mhe. Naibu Spika ameambatana na viongozi na maafisa mbalimbali, akiwemo Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb.), Mhe. CP. Hamad Khamis Hamad, Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Mhe. Jestas Nyamanga, Balozi wa Tanzania nchini Brussels, pamoja na maafisa kutoka Ofisi ya Bunge, Ubalozi wa Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mikutano hiyo inatarajiwa kujadili masuala mbalimbali yenye umuhimu kwa maendeleo ya Afrika na ushirikiano wa kimataifa, ikiwemo amani na usalama barani Afrika, changamoto za migogoro katika baadhi ya nchi za Afrika, madini muhimu (critical minerals), pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wa OACPS.
Kupitia ushirikiano kati ya OACPS na Umoja wa Ulaya, Tanzania imeendelea kunufaika katika maeneo mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo upatikanaji wa misaada na uwezeshaji wa kifedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu, kilimo, uvuvi, madini, biashara na maendeleo ya sekta binafsi. Aidha, Tanzania imenufaika kupitia programu za kikanda chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), pamoja na kupanuka kwa fursa za biashara katika soko la Ulaya na kuimarika kwa ushirikiano katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi, afya, usalama na maendeleo endelevu.
Mikutano hiyo ina umuhimu wa kipekee kutokana na kufanyika kwake baada ya kuanza kutumika rasmi kwa Mkataba wa Samoa wa mwaka 2023, uliochukua nafasi ya mfumo wa zamani wa ushirikiano kati ya ACP na Umoja wa Ulaya. Kupitia mfumo huo mpya, Tanzania na nchi nyingine za Afrika zinatarajia kuimarisha ushirikiano wa maendeleo, biashara, uwekezaji na diplomasia na Jumuiya ya Ulaya kwa manufaa ya wananchi wake.
_1000_666shar-50brig-20.jpg)