Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ufalme wa Eswatini mwenye makazi yake nchini Msumbiji, Mhe. CP. Hamad Khamis Hamad, amewasilisha rasmi Hati za Utambulisho kwa Mtukufu Mfalme Mswati III katika hafla iliyofanyika katika Kasri ya Kifalme, Ezulwini.

Mara baada ya hafla hiyo inayomruhusu kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake ya kidiplomasia nchini humo. Mheshimiwa Balozi Hamad alipata fursa ya kufanya mazungumzo ya faragha na Mfalme Mswati III, ambapo aliwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Katika mazungumzo hayo, alisisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania kuendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria na urafiki uliopo kati ya Tanzania na Eswatini kupitia ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji, utalii, elimu, utamaduni, kilimo na maendeleo ya watu.

Aidha, Balozi Hamad alieleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Eswatini ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na majukwaa mengine ya kikanda na kimataifa kwa lengo la kuimarisha amani, usalama na maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Mfalme Mswati III alimkaribisha rasmi Balozi Hamad nchini Eswatini na kumpongeza kwa kuaminiwa na Rais Samia kuiwakilisha Tanzania. Aliahidi ushirikiano kamili wa Serikali ya Eswatini katika utekelezaji wa majukumu yake na kusisitiza umuhimu wa kupanua ushirikiano wa nchi hizo mbili, hususan katika sekta ya utalii na maeneo mengine yenye maslahi ya pamoja kwa ustawi wa wananchi wa mataifa hayo mawili.