Sambamba na ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Maputo (FACIM 2026), Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), umefanya tukio maalum lililopewa jina la Tanzania Day. Tukio hilo limelenga kutangaza fursa za biashara, uwekezaji, utalii, ubunifu na bidhaa mbalimbali za Tanzania, sambamba na kuimarisha diplomasia ya kiuchumi kati ya Tanzania na Msumbiji.
Hafla maalum iliyofanyika katika banda la Tanzania katika Maonesho hayo, viongozi mbalimbali wa Serikali ya Msumbiji, Mabalozi na Wawakilishi wa Mabalozi kutoka nchi mbalimbali, wakiwemo Balozi wa Rwanda nchini Msumbiji, Kanali Mstaafu Mhe. Donat Ndamage; Balozi wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. J.T. Pitswane; Mwakilishi wa Balozi wa India; Mhe. Balozi wa Mauritius, pamoja na wafanyabiashara kutoka Tanzania na Viongozi wa Diaspora ya Tanzania nchini Msumbiji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. CP. Hamad Khamis Hamad, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji, alieleza kuwa Tanzania Day siyo tu sherehe ya utambulisho wa Taifa, bali pia ni sehemu ya utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi, inayolenga kuunganisha wafanyabiashara, wawekezaji, taasisi na masoko.
Pamoja na masuala mengine, Mhe. Balozi CP. Hamad alisisitiza umuhimu wa Tanzania na Msumbiji kuendelea kubadili urafiki na mshikamano wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizi mbili kuwa ushirikiano imara wa kiuchumi, hususan katika biashara, uwekezaji, kilimo na uongezaji thamani, uzalishaji, utalii, nishati, teknolojia, usafirishaji wa abiria na mizigo, biashara ya mipakani pamoja na ubunifu.
Kadhalika, alieleza kuwa mafanikio ya ushiriki wa Tanzania katika FACIM hayapaswi kupimwa kwa idadi ya wageni wanaotembelea Banda la Tanzania au vipeperushi vinavyogawiwa pekee, bali kwa mahusiano ya kibiashara yatakayojenga, ubia utakaoanzishwa, uwekezaji utakaojitokeza, ajira zitakazozalishwa na manufaa ya pande zote mbili baada ya maonesho hayo.
Moja ya vivutio muhimu vya Tanzania Day ilikuwa sehemu maalum ya “Taste of Tanzania”, ambapo wageni walipata fursa ya kuonja na kufahamu ubora wa kahawa, chai na korosho zinazozalishwa Tanzania.
Akizungumzia tukio hilo, Mhe. Balozi CP. Hamad alieleza kuwa nyuma ya kila kikombe cha chai au kahawa kuna hadithi ya wakulima, wajasiriamali, wachakataji, wafanyakazi, wasafirishaji na masoko, hivyo kuwa na fursa kubwa ya kujenga mahusiano ya kibiashara na uwekezaji.
Vilevile, alitoa wito kwa wafanyabiashara wa Tanzania kutumia fursa zinazopatikana nchini Msumbiji kwa kuelewa soko, mahitaji ya walaji, mazingira ya udhibiti, kutoa bidhaa zenye ubora na ushindani, kujenga uaminifu na kufuatilia kwa karibu mahusiano ya kibiashara yaliyoanzishwa wakati wa maonesho.
Akihitimisha hotuba yake, Mhe. CP. Hamad alisisitiza kuwa Tanzania na Msumbiji zina msingi imara wa kihistoria, kijiografia na kisiasa ambao unapaswa kutumika kujenga mustakabali wa pamoja wa kiuchumi.
Wageni waalikwa pia walipata fursa ya kutembelea Banda la Tanzaniana kujionea bidhaa, huduma na ubunifu mbalimbali unaowakilisha uwezo wa Tanzania katika sekta za kilimo na uchakataji wa bidhaa za kilimo, mifugo, nguo na mitindo, sanaa na ufundi, teknolojia na ubunifu, pamoja na bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wadogo na wakati (SMEs).
Kadhalika, wawakilishi wa taasisi na kampuni zinazoshiriki katika Maonesho hayo walipata fursa za kufanya uwasilishaji na kueleza kwa kina kuhusu taasisi na kampuni zao na lengo mahsusi la kushiriki katika Maonesho hayo.
Kwa ujumla hafla hiyo imeibua muamko mkubwa miongoni mwa watazamaji na wageni wanaotembelea banda la Tanzania kwakuwa na taasisi zinashiriki katika Maonesho hayo zimeonekana kuhitajika kwa kiasi kikubwa nchini humo na hata kwa washiriki wa Mataifa mengine hususan katika suala la uvumbuzo wa telnolojia.
_1000_666shar-50brig-20.jpg)
_1000_666shar-50brig-20.jpg)
_1000_666shar-50brig-20.jpg)
_1000_666shar-50brig-20.jpg)
_1000_666shar-50brig-20.jpg)