Mhe. CP. Hamad Khamis Hamad, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji, ameshiriki katika hafla ya utiaji saini wa Mkataba wa Utekelezaji wa Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Bonde la Mto Ruvuma (Strengthening Integrated Transboundary Source-to-Sea Management of the Ruvuma River Basin and its Coastal Zones to Ensure Ecosystem Health and Livelihood Security) unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania, Msumbiji na Malawi.
Mkataba huo umesainiwa tarehe 31 Julai 2026 ambapo kwa upande wa Tanzania umesainiwa na Mhe. Jumaa Hamidu Aweso (Mb.), Waziri wa Maji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kushirikiana na Mawaziri na wawakilishi wa sekta husika kutoka nchi washiriki.
Mradi huo wenye thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 7.12 na kufadhiliwa na Global Environment Facility (GEF), utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kwa lengo la kuimarisha usimamizi jumuishi wa Bonde la Mto Ruvuma na maeneo yake ya pwani.
Mradi huu unalenga kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za maji, kulinda mazingira, kuongeza ustahimilivu wa jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kukuza fursa za kiuchumi zinazotegemea maji ikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi.
Aidha, ushirikiano huu ni hatua muhimu katika kuimarisha mahusiano ya Tanzania, Msumbiji na Malawi kupitia uratibu wa pamoja katika usimamizi wa rasilimali zinazovuka mipaka, kubadilishana taarifa na uzoefu, pamoja na kuendeleza amani, usalama na mshikamano wa kikanda ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Kabla ya tukio hilo, tarehe 30 Julai 2026 Mheshimiwa Balozi alimpokea na kumkaribisha Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso (Mb.), Waziri wa Maji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyefika Mkoa wa Cabo Delgado kwa ziara ya kikazi akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji pamoja na maafisa wengine.
Ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji unaendelea kuratibu na kuwezesha ushirikiano wa sekta mbalimbali kati ya Tanzania na Msumbiji kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizi mbili.
#TanzaniaMozambiqueRelations #RuvumaRiverBasin #WaterDiplomacy #RegionalCooperation #SADC #TanzaniaDiplomacy
_1000_625shar-50brig-20.jpg)
_1000_625shar-50brig-20.jpg)
_1000_625shar-50brig-20.jpg)