Mhe. CP. Hamad Khamis Hamad, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji, ametembelea Hospitali ya Mkoa wa Cabo Delgado nchini Msumbiji. Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa afya kati ya Tanzania na Msumbiji.

Akiwa hospitalini hapo, Mhe. Balozi alipokelewa na uongozi wa Hospitali pamoja na viongozi wa sekta ya afya wa Mkoa wa Cabo Delgado, na kupata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya hospitali ikiwemo mapokezi ya wagonjwa, vyumba vya uchunguzi na uangalizi wa wagonjwa mahututi, Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU), maabara, pamoja na kitengo cha uchunguzi wa mionzi.

Pamoja kutembelea maeneo yaliyoainishwa, Mhe. Balozi alifanya mazungumzo na uongozi wa Hospitali, ambapo pamoja na masuala mengine walijadili changamoto za baadhi ya vifaa tiba na wataalamu wa kutafsiri vipimo vya mionzi. Aidha, baadhi ya vipimo vya CT Scan hulazimika kupelekwa katika Mkoa mwingine kama Nampula kwa uchambuzi, hali inayoweza kuchelewesha huduma kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya haraka.

Kufuatia mazungumzo hayo, Mhe. Balozi alieleza umuhimu wa kuendeleza urafiki na mshikamano wa kihistoria kati ya nchi hizi mbili kwa kupeleka ushirikiano huo katika sekta zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, hususan afya.

Aidha, Mhe. Balozi aliwasilisha wazo la kuanzisha Tanzania–Mozambique _Medical Outreach and Friendship Mission_, mpango unaolenga kuleta timu ya wataalamu kutoka Hospitali Bingwa ya Benjamin William Mkapa (BWMH) kutoa huduma za matibabu na uchunguzi wa magonjwa mbalimbali bila malipo kwa wananchi wa Cabo Delgado baada ya kukamilika kwa taratibu za maandalizi.

Vilevile, alipendekeza kuanzishwa kwa ushirikiano wa kitaasisi kati ya Hospitali ya Mkoa wa Cabo Delgado na hospitali za Tanzania ikiwemo BWMH, Muhimbili na Mloganzila kupitia mabadilishano ya wataalamu, mafunzo na kubadilishana uzoefu.

Uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Cabo Delgado ulipokea kwa moyo mkunjufu mapendekezo hayo na kuonesha utayari wa kushirikiana na taasisi za afya za Tanzania.

Ziara hii ni sehemu ya juhudi za Ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji kuendeleza diplomasia ya afya (Health Diplomacy) na kuimarisha mahusiano ya kihistoria kati ya Tanzania na Msumbiji kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizi mbili.