Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji, ukiongozwa na Mhe. CP. Hamad K. Hamad, Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, umeshiriki katika Kongamano la Utalii na Uwekezaji la Msumbiji (Mozambique Tourism & Investment Forum 2026) lilikofanyika kuanzia tarehe 3 hadi 6 Juni, 2026 katika Mkoa wa Nampula.Lengo kuu la kongamano hilo ni kujadili namna ya kuimarisha mchango wa sekta ya utalii katika maendeleo ya uchumi na kuvutia uwekezauji nchini Msumbiji.

Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mhe. Basílio Muhate, Waziri wa uchumi wa nchi hiyo ambaye ndiye alikua mgeni rasmi. Washiriki wengine ni pamoja na Mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao nchini Msumbiji, wawakilishi kutoka nchi kadhaa ikiwemo Tanzania, Zanzibar, Mauritius, Ghana, Kenya na Malawi, wawekezaji, taasisi za maendeleo, wataalamu wa utalii na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya Msumbiji.

Dhima kuu katika kongamano hilo ni
“Kuiweka Msumbiji kama Kituo Kinachoshindana Kimataifa katika Utalii na Uwekezaji kupitia Utalii Endelevu, Uboreshaji wa Miundombinu na Ushirikiano wa Kikanda.”

Kongamano hilo lilihusisha mijadala mbalimbali kuhusu mikakati ya kuiwezesha Msumbiji kuwa kitovu cha utalii na uwekezaji katika ukanda wa Kusini mwa Afrika kupitia utalii endelevu, maendeleo ya miundombinu, ujenzi wa chapa ya taifa (National branding) na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

Katika hotuba yake, Waziri Muhate alisisitiza umuhimu wa kuwa na mikakati madhubuti ya kujenga sekta ya utalii endelevu kupitia uwekezaji katika miundombinu, kuimarisha muunganiko (connectivity) wa huduma za usafiri wa anga, baharini na nchi kavu, pamoja na kuendeleza utalii wa kisasa (modern tourism) unaoendana na mahitaji ya wakati na mabadiliko ya teknolojia.

Kwa ujumla, ushiriki wa Ubalozi wa Tanzania katika Kongamano hilo umetoa fursa muhimu ya kujifunza uzoefu wa Msumbiji na nchi nyingine kuhusu matumizi ya utalii kama nyenzo ya maendeleo ya uchumi, uwekezaji na ushirikiano wa kikanda.

Aidha, kongamano hilo linaweka wazi umuhimu wa kuendelea kuimarisha juhudi za ndani kwa kila nchi ikiwemo Tanzania katika kujitangaza kimataifa, kuvutia uwekezaji, kujenga ushirikiano wa kiuchumi na kuendeleza sekta ya utalii kama kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa Taifa.